Pd. Laurenti C. Magesa alikuwa ni mmojawapo wa wawezeshaji katika semina elekezi ya Sinodi ya Jimbo. Katika semina hiyo, alitoa mada kuhusu Sinodi katika Historia ya Kanisa.
Ifuatayo ni mada aliyoitoa kama ilivyokaririwa na Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Maandalizi ya Sinodi.
Sinodi haizungumzii tu mambo yetu ya Musoma jimboni ila inatusaidia:
· Kukua upya kama wakristo katika imani na matendo. Alitoa pongezi kwa kamati iliyobuni kauli mbio ya Sinodi “SINODI MUSOMA, IMANI NA MATENDO” na kusisitiza kuwa imani bila matendo imekufa.
· Kujenga umoja wa Kanisa KOINONIA. Umoja huu kati yetu wakristo unatusaidia kuwa na mshikamano ili tusije tukajikuta tumesambaratika.
· UPENDO. Palipo na upendo hapo Mungu yupo kwa sababu Mungu ni upendo. Akirejea Maandiko Matakatifu, kitabu cha Matendo ya Mitume 2: 42-26, alisisitiza kuwa amri iliyo kuu ni ile ya upendo. Wakristo wa kwanza walitambulikana kwa sababu ya upendo waliokuwa nao, hata kufikia watu wengine kusema kuwa angalieni wanavyopendana.
· AMANI. Palipo na amani pana upendo, pasipo amani hakuna upendo. Katika mchakato wa Sinodi tulenge katika kujenga amani. Pamoja na kuwa waamini, bado kati yetu matatizo yanatokea. Jambo la muhimu ni kuangalia kwamba ni namna gani basi tunavyoyakabili matatizo yanayotokea kati yetu. Kwani ni jambo la kawaida kabisa kuwa tunapoishi tunajikuta katika matatizo mbalimbali yenye kuleta hata migongango kati yetu.
SINODI KATIKA HISTORIA YA KANISA
Alieleza kwamba Kanisa katika mitaguso mbalimbali limejaribu kutatua matatizo yaliyojitokeza kwa nyakati zake. Alisema swala muhimu ni kwamba tunasuluhisha na kutatua namna gani matatizo hayo tanayotupata katika safari nzima ya uinjilishaji. Mitaguso imetumika katika kutatua matatizo mengi ambayo Kanisa limekutana nayo katika vipindi mbalimbali. Alitoa mfano wa Mtaguso wa Yerusalemu (mwaka 48-49 BK) kwamba huu ulikuwa wa kutatua tatizo la tohara kwa waliotaka kuingia katika ukristo ambao hawakuwa Wayahudi. Mtume Petro katika kueleza suluhu alisema Roho Mtakatifu na sisi tumeamua kuwa tohara siyo ya lazima kwa wale wasio Wayahudi. Padre Magesa alisisitiza kuwa ni swala la msingi kabisa kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu katika mijadala ya Sinodi na katika kufikia maamuzi. Akirejea Maandiko katika kitabu cha Matendo ya Mitume 15:6-29, katika kutatua swala la tohora katika Kanisa la awali, alisema haikuwa lazima kufuata mila za kiyahudi katika swala la tohara. Pia alisisitiza kuwa kuwa tusije tukajikita zaidi katika kufuata mila na tamaduni zetu na kusahau nguvu ya Roho Mtakatifu anayeliangazia na kuliongoza Kanisa.
Baada ya Mtaguso wa Yesusalemu, kumekuwako mitaguso mbalimbali ya Kanisa. Alieleza kuwa tofauti kati ya Mtaguso na Sinodi ni kwamba Mtaguso unajumuisha Kanisa zima wakati Sinodi inajumuisha Kanisa mahalia (jimbo) yaani sehemu tu ya Kanisa zima. Akitolea mfano wa Mtaguso wa Nicea wa Mwaka 325 BK, alisema Mtaguso huu umetupatia Kanuni ya Imani kwa sababu swala kubwa lililojadiriwa liligusa tatizo lililokuwapo kwamba Yesu ni Mungu au la? Awali walitokea wazushi waliodai Yesu hana umungu ila ni binadamu tu. Ndipo Kanuni ya ungamo la imani ikaweka wazi kuwa Yesu ni Mungu sawa na Baba na Roho Mtakatifu katika umoja.
Kuhusu Mtaguso wa pili wa Vatikano 1962 hadi 1965, alieleza kuwa umeleta mabadiriko makubwa sana ndani ya Kanisa. Hati 16 za Mtaguso wa Pili wa Vatikano ni za muhimu sana katika kutupatia mwelekeo wa Sinodi yetu ya jimbo la Musoma. Alieleza kuwa ni bahati mbaya sana kwa vile imebainika sehemu nyingi sana kwamba watu wengi hawazijui hati hizi na wala hakuna mikakati ya kuzifanya zifahamike wa watu wengi zaidi. Akieleza zaidi kuhusu Mtaguso wa pili wa Vatikano alisema:
· Mtaguso wa pili wa Vatikano ulikuwa zaidi na sura ya kichungaji totauti wa ule wa Trenta wenye matamko mengi ya anathema, yaani alaaniwe. Yaani matamko mengi ya kulaani na kuwatenga na umoja wa Kanisa wale wote waliofikiri kinyume na mawazo ya Kanisa. Mtaguso wa Pili wa Vatikano haukuwa wa kuwajengea watu uoga wa sheria ila kuwafanye waelewe na kuwa huru kujieleza katika mijadala inayolenga katika kufikia maelewano. Hiyo ndio tofauti kati ya Mtaguso wa pili wa Vatikano na ile iliyotangulia.
· Ndani ya Kanisa Barani Afrika, Mtaguso wa pili wa Vatikano umezaa Sinodi mbili, ile ya mwaka 1994 na ya mwaka 2009. Ni bahati kwamba Kanisa barani Afrika limepata Sinodi mbili baada ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano, tofauti na mabara mengine. Hii ni ishara wazi ya kwamba Kanisa barani Afrika linakuwa na kuongezeka. Miito inapungua sehemu nyingi, ambapo barani Afrika miito inaongezeka na hali kadhalika wamisionari wa kutoka barani Afrika wanaongezeka na kwenda kuinjilisha katika sehemu nyingi za ulimwengu.
· Padre Laurenti alisisitiza kuwa hatuwezi kufanikiwa katika Sinodi yetu ya sasa ya jimbo la Musoma bila kuzifahamu na kufanya rejea katika Sinodi hizo mbili zilizotangulia yaani ile ya mwaka 1994, iliyohusu uinjilishaji na ile ya mwaka 2009 iliyohusu upatanisho, haki na amani kama nyenzo ya uwajibikaji katika Afrika.
Padre Magesa alisema tunachotaka kupata katika Sinodi yetu ya jimbo la Musoma ni ili kwamba Sinodi:
Mosi: itusaidie kama Kanisa la Musoma kujijenga upya kiroho. Kanisa linahitaji njia za uinjilishaji zinazoendana na wakati huu tulio nao. Kwa mfano, kuna haja ya kuangalia na kubaini kuwa vijana wengi hawaendi maKanisani. Ipo haja ya kuangalia sababu zinazopelekea tatizo la vijana kutojali mambo ya kiroho. Inawezekana mbinu zetu za uinjilishaji hazigusi maisha yao, kwa jinsi hiyo kuna haja zaidi ya kuona namna ya kufanya uinjilishaji mpya kwa vijanana makundi mengine ya watu wa Taifa la Mungu.
Pili: ni kuona jinsi ya kuchangia katika maendeleo ya jamii ambayo tunaishi na kuihubiria, ili kuifanya ijikomboe kiuchumi, kiafya na kielimu. Akiwasifu wamisionari wa shirika la Maryknoll, Padre Magesa alisema walifaulu kuinjilisha jimboni Musoma kwa sababu pia waliweka miundo mbinu ya kuwapatia watu elimu na afya. Kila walipojenga Kanisa, walijenga pia shule na zahanati. Huo ni ushahidi ulio wazi kwani wengi wa umri wake waliopo katika semina hiyo wemepitia shule za Kanisa.
Tatu: ni kuishi imani yetu kulingana na alama za nyakati, yaani kuishi maisha yetu kufuatana na alama za nyakati. Kanisa ni chombo cha kichungaji na hivyo yatupasa kuliona Kanisa kuwa ni mwili wa Kristo kwa karama mbalimbali. Ni lazima kushirikisha karama katika Sinodi. Ni dhambi kubwa kabisa kuzima karama ya mtu aliyopewa na Roho Mtakatifu. Pengine vile viungo tunavyoviona kuwa dhaifu sana ni vya maana sana katika mwili. Hali kadhalika inawezekana kuna watu tunaowaona kuwa dhaifu sana, hao ni wa maana sana katika Kanisa.
Padre Magesa alisema kwamba mchango mkubwa sana ulitokana na ile Sinodi ya kwanza ya Afrika, iliyosema Kanisa ni familia ya Mungu inayotembea pamoja, na ile ya pili inayozungumzia haki, amani na upatanisho katika kuwajibika. Alisisitiza umuhimu wa familia katika kuyajua na kuyaishi maadili ya kimungu. Ni namna gani tunaweza kuyaishi maadili ya Mungu katika jumuiya zetu bila kuyajua? Alisema ni lazima tuangalie watu wa mahali fulani wanafanyaje. Hivyo Sinodi ijadili na kuona ni sera ipi ya jimbo letu tunayoihitaji. Kumbe sera hiyo ni lazima ijulikane kwa sababu sera isiyojulikana haina faida kuwapo. Akitolea mfano wa taa alisema taa inapowashwa ni lazima iwekwe katika kinara ili umulike na kutoa mwanga. Tuangalie mbinu gani zitumike katika kukabiliana na changamoto za kichungaji tulizo nazo. Kuna hazina nyingi tunaweza kupata za kutusaidia kuwa na sera za jimbo letu zilizo na mafaa katika kazi ya uinjilishaji. Kuna mila ambazo zimekuwapo katika jamii yetu kwa miaka mingi na watu wameishi kwa kulindwa na maadili yanayotokana mila hizo. Walioziweka hawakuwa wajinga, ila waliona zinawafaa. Hivyo ni vema kuzungumza nao ili kuona ni tunu gani zinaweza kutokana na mila hizo zinazoweza kusaidia uinjilishaji. Haitoshi kwa mfano Padre akawaambia watu kuwa mila zenu ni mbaya na ni lazima kuachana nazo. Akifanya hivyo bila kujua undani wake, watu watasema tu mbele yake “ndio Padre tumeacha” wakishampa tu mgongo wanaendelea kufanya kama walivyozoea. Pengine mara kadhaa imeonekana kwamba katika Kanisa kuna tunu zimepungua hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya mila ambazo zimekuwa na faida katika jamii kwa muda mrefu. Kuna haja ya kushirikishana ili kuzibaini tunu hizo zinazopungua. Mara nyingi utakuta Paroko ameonekana kuachiwa mambo yote, ni wazi kuwa hawezi kuyafanya. Mshikamano unaojikita katika kushirikishana utalisaidia Kanisa jimboni Musoma kufaidi matunda ya Sinodi tuliyoianza. Sinodi haitaisha itakapofika mwishoni mwa mwaka kesho ila itaendelea kuwa sehemu ya maisha ya watu wa Mungu jimboni Musoma.
Akizungumzia kuhusu swala na maendeleo alisema ni lazima kuona kuwa kuna mipango endelevu ya kuleta maendeleo kuanzia katika parokia. Kuna mabaraza yapo, ya walei, ya kichungaji, na vyombo mbalimbali vya kutekeleza mipango hiyo. Tuna wajibu wa kuishi maisha ya kujitegemea na kutumia kile tulicho nacho. Waafrika tuna msemo “Mimi sili kwako” maana yake ninajitegemea, ninakula jasho langu. Tutambue kuwa hatuwezi kuwa tunategemea ufadhili wa wageni toka nchi za nje. Kuna mengi ambayo tunaweza kuyafanya yakatupatia hata kama ni kidogo lakini cha kwetu ambacho tunaweza kujivunia na kukitegemea. Cha kupewa au cha kuomba hatuwezi kukitegemea kwa sababu hatujui ni lini kipo na lini hakipo.
Alisema Sinodi ni jambo/mkutano mtakatifu na ni jambo lenye kuja baada ya uamuzi/maamuzi makubwa sana. Hili linakuja kwa sababu kubwa sana ambazo zinamfanya Baba Askofu akafikia uamuzi wa kuanzisha mchakato wa Sinodi ya jimbo la Musoma. Sababu hizi amezieleza vizuri sana jana katika hotuba ya ufunguzi.
Kuna wajibu wa kila mmoja kuchangia katika Sinodi hii, kwa ajili ya kulinda heshima na sifa yetu pia na sifa ya kila mmoja huku akizingatia kuwa mkweli mbele ya Mungu na mbele ya wenzake. Maazimio na maamuzi yatakayotokana na Sinodi yakishapitishwa, yakaidhinishwa kwa kuwekewa sahihi na Baba Askofu, yanabaki kuwa siyo mali yetu tena waamini wa Musoma tu bali inakuwa ni mali ya Kanisa zima la ulimwengu. Yaliyomo sasa yatafanyiwa rejea na wengine wa majimbo ya nje kama Mwanza, Geita au kwingineko. Yaliyomo ni waraka wa Kanisa zima.
Padre Laurenti alimalizia kwa kutoa tahadhari katika mambo yafuatayo:
· Kwamba hatuwezi kufikia maamuzi sahihi tusipoelewa mambo vizuri. Alisema imani inatafuta kuelewa, hivyo siyo busara na haikubaliki watu kuburuzwa katika mijadala ila wajadili mambo kwa uhuru kamili. Akitolea mfano wa Katekisimu ya Kanisa Katoliki alisema ni ya uinjilishaji na siyo ya kukaririshw bali kuelewa na kuyaishi yaliyomo.
· Kuzingatia mabadiriko katika Kristo. Kanisa ni mwili hai ambao usipobadirika unakufa. Kanisa la leo siyo lile na 1947 hivyo kwa kila namna ni lazima tukubali kubadirika.
· Tukumbuke la muhimu ni kwamba tuwe na SINODI BORA NA SIYO BORA SINODI. Tunategemea mchango wa kila mmoja na jambo la muhimu ni kujenga mahusiano yetu vizuri na Kristo. Kwa hiyo tutajikuta tunakuwa watu wenye mahusiano mazuri na Kristo.
Padre Magesa alimaliza kwa kuwashukuru wajumbe wote wa semina kwa ushiriki na michango yao na kuwahimiza kuwashirikisha watu wote wa Taifa la Mungu matunda yatakayotokana na sinodi ya Jimbo la Musoma.
No comments:
Post a Comment