Mh. Baba Askofu Michael Msonganzila ametoa barua ya kutangaza ufunguzi rasmi wa Sinodi ya Jimbo. Barua hiyo iliyotolewa tarehe 5 Mei 2013 imethibitisha kuwa ufunguzi huo utafanyika siku ya Pentekoste tarehe 19 Mei 2013. “Misa itafanyika katika makao makuu ya Jimbo, yaani Parokiani Musoma Mjini katika viwanja vya Matumaini katika Vijana kuanzia saa 4:00 asubuhi. Misa itaongozwa nami Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila”, ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Itakumbukwa kuwa ni katika viwanja hivyo Baba Askofu alitangaza kwa mara ya kwanza nia ya kuitisha Sinodi ya Jimbo. Tangazo hilo alilitoa tarehe 3 Oktoba 2011 katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Ukristo Jimboni. Viwanja hivyo vitawapokea tena waamini kutoka kila pembe ya Jimbo letu katika tukio kubwa la ufunguzi wa Sinodi wiki mbili zijazo.
Katika barua hiyo Baba Askofu alieleza pia kuwa ndani ya adhimisho la Misa ya ufunguzi atawaapisha wawakilishi wote aliowateua kushiriki mikutano mikubwa ya Sinodi. Wawakilishi hao “wataapishwa kwa sababu tendo la maadhimisho ya Sinodi ni tendo la Imani Katoliki”, alieleza.
Siku hiyo kutakuwa na Misa Moja tu katika Jimbo zima. Kwingineko maparokiani, hasa parokia zilizo nje ya udekano wa Musoma Mjini, ruhusa ya pekee imetolewa kwa Mapadre kusali Misa ya Kesha la Pentekoste Jumamosi jioni tarehe 18 Mei. Watashiriki Misa ya kesha hasa wale ambao hawatapata bahati ya kushiriki Misa ya Jumapili ya Pentekoste Musoma. Aidha, Makatekista wataongoza Ibada ya Dominika bila Padre siku ya Jumapili kwa wale ambao hawakushiriki Misa ya Kesha.
“Nawatakia maandalizi mema ya matukio hayo muhimu yaliyoko mbele yetu yanayogusa uhai na ustawi wa Jimbo letu la Musoma” alihitimisha Baba Askofu.
No comments:
Post a Comment