Jimbo na Historia Yake

 JIMBO LA MUSOMA NA WATU WAKE

JIOGRAFIA YA JIMBO KATOLIKI LA MUSOMA
Kabla ya kuundwa kwa Jimbo Jipya la Bunda, Novemba 27, 2010, Jimbo la Musoma lilikuwa na mipaka ya ukubwa sawa na ile ya Mkoa mzima wa Mara – ambao uko Kaskazini mwa Tanzania. Kwa sasa, Jimbo la MUSOMA linapakana na majimbo ya Bunda (lililozaliwa toka Musoma na Mwanza), upande wa kusini Arusha na nchi ya Kenya upande wa mashariki. Sehemu kubwa ya upande wa Mashariki mwa Jimbo zinakutwa mbuga za wanyama za Serengeti ambapo jimbo la Musoma linapakana na majimbo ya Shinyanga na Mbulu. Kwa ukubwa, kwa sasa (tukiondoa Jimbo la Bunda), Jimbo la Musoma linakadiriwa kuwa na ukubwa wa Kilomita za Mraba zipatazo 24,019.
WAKAZI WA MKOA WA MARA
Hadi kufikia Mwaka 2004, idadi ya wakazi wa Mkoa wa Mara ilikuwa ni takribani watu wapatao 1,400,000 na kati ya hao watu takribani 260,000 wakiwa ni wakazi wa Wilaya ya Bunda. Idadi ya Wakatoliki ilikuwa ni takribani watu 250,000 sawa na asilimia 17.9. Kwa upande wa makabila yanayokutwa Mkoa wa Mara, yako mengi. Baadhi ya hayo ni yafuatayo: Waluo, Wajita, Waruri, Wazanaki, Wakurya, Wakabwa, Wakiroba, Wasimbiti, Wangoreme, Wakwaya,Waikoma, Wanata, Waisenye, Waikizu na Walieri.
MAISHA YA IMANI KABLA YA UJIO WA WAMISIONARI
Kama tunavyojifunza kutoka katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki kuwa, tamaa na kiu ya Mungu imeandikwa na Mungu mwenyewe ndani ya kila mwanadamu (Katekisimu ya Kanisa Katoliki. n. 27 - 28) hali kadhalika, kabla ya Ujio wa Wamisionari, wenyeji wa Mkoa wa Mara nao walionesha kiu yao kwa namna mbalimbali.

Wenyeji wa Mkoa wa Mara, tangu zamani walikuwa na Imani zao za jadi, kuheshimu (au kuabudu) jua na viumbe vingine kama vile miti mikubwa, miamba, mapango, mito mikubwa, majoka makubwa, na viumbe vingine kama hivyo. Hali kadhalika wapo walioamini katika uchawi na ushirikina, kupiga ramli, matambiko, mazindiko, mizimu, na mambo mengi tu ya giza. Walitafuta majibu ya maswali yao magumu kutoka katika nguvu hizi.

Hivyo, haikuwa rahisi kwao kubadilika na kuupokea ukristo mara moja na kwa urahisi, na hata baadhi ya wale waliopokea Imani ya Kikristo walijikuta wanashindwa kubandukana na imani yao ya jadi, na kuishia kuchanganya yote mawili, Ukristo na Imani za jadi (syncretism), hali ambayo bado ipo hadi leo hii katika baadhi ya maeneo.

Sambamba na imani za namna hiyo (kama zilivyotajwa hapo juu), bado pia walikuwa na mila na desturi zingine ambazo ni kinyume cha Ukristo, kama vile, kuoa wake wengi, kutupa watoto waliozaliwa mapacha, nyumba ntobhu (katika jamii za Wakurya), kurithi wajane (katika jamii za waluo).

Hii ndiyo ilikuwa picha ya jumla katika jamii za wenyeji wa Mkoa wa Mara kuhusiana na suala zima la imani zao kabla ya ujio wa wamisionari.

Ramani ya Jimbo Katoliki la Musoma na Bunda


UJIO WA WAMISIONARI

Huku wakisukumwa na Agizo la Kristo kwa Mitume wake: “Enendeni ulimwenguni mwote mkawafanye Mataifa yote kuwa wanafunzi wangu…” (Mt. 28:19), wamisionari wa makundi mbalimbali wanajitokeza kuendeleza kazi ambayo Kristo mwenyewe aliifanya, na baadaye kuikabidhi kwa Mitume wake ili kuiendeleza, kwa njia ya Kanisa – ambalo kwa asili yake ni la kitume (missionary). Wanaitikia Mwaliko wa Kristo: “nanyi mtakuwa mashahidi wangu” (Mate. 1:8) na kwa msukumo huo wa kiimani, wanafika maeneo mbalimbali ya ulimwengu, ikiwemo Afrika na kwa namna ya pekee, maeneo ya Mkoa wa Mara sasa takribani miaka 100 iliyopita. Ni Neno la kumshukuru Mungu, ambaye karne hata karne haachi kuwainua watu ambao wako tayari kumtangaza kwa mataifa yote.

Wamisioari waliofika katika maeneo ya Mkoa wa Mara, wako katika makundi makubwa mawili: Mapadri Wamisionari wa Afrika na Mapadri na Watawa wa Shirika la Maryknoll

SHIRIKA LA MAPADRI WAMISIONARI WA AFRIKA (WHITE FATHERS)
Wamisionari wa kwanza kabisa kuleta Imani ya Kikristo katika maeneo ya Mkoa wa Mara ni Mapadre wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers). Shirika hili lillianzishwa na Kardinali Lavigerie aliyekuwa Askofu wa Algiers.
Wamisionari hawa walifika katika kanda ya ziwa Victoria tarehe 24 Desemba 1878 wakitokea Bagamoyo na walifikia Malya. Katika siku hiyo waliadhimisha hapo Malya Misa ya sherehe ya Krismasi. Baada ya kutoka Malya walielekea Uganda. Mwaka 1883 waliondoka Uganda wakaenda Bukumbi. Hapo Bukumbi pakawa makao yao makuu kwa kanda ya ziwa. Kutoka Bukumbi wakaanza kusambaa kimakundi. Kundi la kwanza lilielekea Kagunguli na kundi la pili likaelekea Kome. Kundi lililoelekea Kagunguli ndilo lililofika maeneo ya Mara.

Siku za kwanza kwanza baada ya kufika Afrika hazikuwa rahisi kwani walikutana na changamoto nyingi, zikiwemo zile zilizowakumba wenyeji, au wao wenyewe. Kwa wakati huo, changamoto kubwa ambayo walipambana nayo ni BIASHARA YA WATUMWA – iliyokuwa ikifanywa na Waarabu.

JITIHADA ZA MWANZO ZA UINJILISHAJI ZA WAMISIONARI WA AFRIKA

Mnamo Mwaka 1895 ndipo ilipojengwa Misioni ya Kagunguli na mapadre waliotokea Bukumbi wakipitia Mwanza. Wamisionari hao walipofika Bukumbi walitamani kufika maeneo ya Bara – yaani Mara hasa maeneo ya WAJITA na WARURI, azma ambayo ilitimia baadaye.
Chini ya maelekezo na maongozi ya Askofu Jean Hirth, wamisionari hao walitumwa na Askofu wao toka Kagunguli na kufika maeneo ya Bururi, mapadri wa kwanza wakiwa ni Joseph Van Thuet na Henry Van Thiel wa White Fathers. Wakiwa safarini walipitia maeneo ya Kisiwa cha Kweru na baadaye kufika Bwasi / Majita (nchi kavu), na hapo Bwasi utume wao ulianza kwa mara ya kwanza bara, na baada ya kukaa kwa muda tu, na kusia mbegu ya Injili hapo na hata kuacha mti wa kumbukumbu, waliendelea mbele na kufika maeneo ya Bukwaya – hasa maeneo ya Nyakatende mnamo mwaka 1897.


Kanisa la sasa la Nyakatende kama lilivyoonekana mwaka 2011 wakati wa ujenzi wake

Walipofika maeneo ya Bukwaya walipokelewa na wenyeji kwa mitazamo tofauti, wachache wakiwakubali na huku wengi wakiwa wazito kuwapokea akiwemo Mtemi wa wakati huo - Nyakuringa ambaye, alikaa maeneo ya Mkirira. Kwa vile Mtemi hakupenda kukaa karibu nao, aliwapa maeneo yasiyofaa ya Nyakatende. Ujumbe wa Mapadre Van Thuet na Thuel na Br. Balthazar wakawa wamefika Nyakatende ambako walipokelewa kwa shida na hata dini yao (ukristo) ikapokelewa kwa shida kwa tafsiri kuwa mambo ya wazungu yalikuwa ya kitoto, kama walivyozoe kusema “amang’ana ga bajungu ga kyana.” Hakika haikuwa rahisi kwa wenyeji waliokuwa na Imani zao za jadi kupokea kirahisi ukristo.

Wakiwa hapo Nyakatende, Wamisionari hao wa kwanza walipata pigo kubwa la kufiwa na mwenzao Pd. Joseph Van Thuet mwaka huo huo wa 1897, kutokana na hali mbaya ya hewa na malaria. Matokeo ya kifo hiki yalikuwa ni kufungwa kwa kazi ya Umisionari maeneo ya Bukwaya kwa amri ya Askofu Jean Hirth, na hapo Pd. Henry Van Thiel na Br. Balthazar wakawa wamerudi Ukerewe, hadi mwaka 1907 ambapo Pd. Van Thiel aliamua mwenyewe kurudi tena na kuendelea na kazi ya Uchungaji katika maeneo ya Bukwaya, akifika hadi Majita, Zanaki, Ngoreme, Ikizu, na baadaye kurudi tena Ukerewe.
KUENDELEA KWA KAZI YA UINJILISHAJI
Mnamo mwaka 1909, Pd. Henry Van Thiel alirudi tena Nyegina akiambatana sasa na Padre mwingine aliyejulikana kama Pd. Embil na Bruda Balthazar. Walipofika na kuona na na Mtemi Nyakuringa, aliwaelekeza sasa wajenge Mkirira, yaani Nyegina ya Garore, ambapo palikuwa pabaya kuliko Nyakatende.

Kwa vile Nyegina ya Garore haikufaa, wamisionari walilazimika kutafuta maeneo mengine ambayo baadaye yalitolewa na wenyeji kama vile Mzee Ryabwere na Mzee Minangi, maeneo ambayo yalitumika kwa ujenzi wa Kanisa, Nyumba ya Mapadre na ya Masista, Zahanati, Shule, eneo la makaburi na la michezo pia. Eneo lingine walilotoa lilitumika kwa ajili ya kilimo cha matunda, migomba na miembe - ambayo huonekana hadi leo hii. Kadiri ya muda upinzani dhidi ya wamisionari ulipungua, na hata wafuasi wakawa wikizidi kuongezeka.

Mnamo mwaka 1911 ndipo ulipoanza rasmi ujenzi wa Kanisa chini ya usimamizi wa Bruda Balthazar akisaidiwa na mafundi wazalendo toka Ukerewe na bara. Kadiri ya muda, afya ya Padri Henry Van Thuel ilizidi kudhoofika kutokana na hali mbaya ya hewa na malaria, na kufuatia hali hiyo, Padri mwingine alitumwa toka Bukumbi kuja Nyegina mnamo mwaka huo huo 1911 ili aje kuwaongezea nguvu wamisionari ambao sasa walikuwa wanaelemewa na kazi. Huyu aliitwa Pd. Tish Kwa bahati mbaya, mnamo tarehe 26.05.1911 Pd. Henry Van Thiel alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alizikwa hapo hapo Nyakatende karibu na Kaburi la mwenzake Pd. Van Thuet.

Baadaye mwaka huo huo, Pd. Tish alirudi Mwanza na wakaletwa Mapadri wengine wawili hapo Nyegina ambao ni Ettiene Brussard na P. Van de Wee. Mapadre hawa walishirikiana vizuri na mwenzao Pd. Embil kueneza Injili ya Kristo. Kadiri ya muda, ukristo ukaenea maeneo mengi na hata Nyegina ikawa sasa kivutio cha watu wa maeneo mengine kama vile Mwisenge, Etaro, Makoko, Mmahare, Busamba, Nyiraegenge, Kigera, Ekungu na kwingineko.

Watu kutoka maeneo hayo yote walikuwa wakija Nyegina kusikiliza Neno la Mungu. Hali hii ilikuwa faraja kwa wamisionari kuwa kazi yao inazaa sasa matunda na hata kusahau taabu na mateso ya kipindi cha nyuma. Kwa kipindi hiki, makao yao makuu yalikuwa ni Nyegina wakati Mkirira, Nyakatende (walikokuwa wameanzia) palibaki kama vigango.

Baada ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya mapadre ya miti, ulianza ujenzi wa Kanisa – kwa ushirikiano kati ya Mhandisi – Br. Balthazar akisaidiwa na mafundi na vibarua wenyeji wakiwemo Ndarira Nkabi, Paulo Nyamswa, Daudi Mkenye na wengineo.

Imani ya Kikristo iliendelea kukua na kuenea mahali pengi, matunda yalianza kuonekana, ambapo Mwaka 1911 June wawili walibatizwa na Pd. D. Embil mmoja wao akiwa ni Joseph Warioba na baadaye akapatikana Katekista wa Kwanza aliyeitwa Silveri Nyakubhoga (aliyekuwa mlemavu asiyeona), na pia mwimbaji maarufu – Mikaeli Kitanda (ambaye naye alikuwa mlemavu asiyeona). Katika mafanikio yote haya, mchango wa pekee wa Pd. Embil utakumbukwa, na hasa jinsi alivyokuwa karibu sana na watu.

Mnamo mwaka 1916 Wamisionari walipanua wigo wa utume wao na kuanzisha pia huduma mbalimbali za jamii kama vile: Shule – ambazo mwanzoni zilianzishwa na Pd. P Van De Wee, na baadaye kuendelezwa na Pd. Schneider aliyefika Nyegina mwaka 1915, akifuatiwa na Pd. Spoto mwaka 1922.

Hadi kufikia mwaka 1930 walikwishaongezeka Mapadre wengi wamisionari – akiwemo: Pd. Rivard, Joseph Barthlomew. Ukristo ulienea na watu wengi zaidi walivutiwa kwenda Nyegina – wengine wao wakitokea mbali.

Kadiri ya muda, na kadiri ya mahitaji ilibidi uanzishwe utaratibu wa kupeleka dini na maeneo mengine, ambalo liliungwa mkono na Pd. Brussad, japo Pd. Van Joseph Bathlomew hakuliunga mkono kwa kiasi kikubwa. Injili ikaendelea kusonga mbele kadiri ya siku.

Kanisa la Nyegina kwa Sasa
SAFARI KWENDA KOWAK
Baada ya maombi ya muda mrefu ya jamii ya Waluo kuomba Wamisionari waende kuinjilisha maeneo ya Waluo, mwishowe ombi lao lilikubaliwa na Pd. Ettiene Brussard aliteuliwa kwenda kuhubiri maeneo ya Waluo, na safari yake ya kwanza ilikuwa mwaka 1928. Msafara huu kwa hakika ulikuwa wa kipekee kwani ulihusisha watu wengi. Kati ya watu hao alikuwamo Bruda Balthazari.

Mnamo mwaka 1929 kibali cha ujenzi wa Kanisa katika jamii ya Waluo kilitolewa, na ujenzi ulianza rasmi hapo Buturi na kukamilika mwaka 1931. Kwa kipindi chote hicho cha ujenzi wa Kanisa, Padri alikuwa akiishi Nyegina wakati Bruda Balthazari alibaki eneo la Buturi kusimamia ujenzi.

Mafundisho ya Dini kwa wakati huo yaliendelea kutolewa hapo Buturi chini ya usimamizi wa Mapadre wakishirikiana na makatekista wawili; Victor Awino na Bernard Akoko – ambaye baadaye aliingiza lugha ya Kiluo katika mafundisho ya dini, baada ya kuwa amepata Mafundisho kwa lugha hiyo toka Kenya.

Makatekista hawa waliwahimiza watu katika kudumu katika maadili mema. Mwaka huo huo wa 1931 Pd. Brussard alihamia Buturi na baadaye kufuatiwa na Pd. William na wote waliishi pamoja na Bruda Balthasar hapo Aheko Buturi. Mwaka 1933 Kituo cha Kanisa la Aheko Buturi kilipata hadhi ya Parokia.

Kadiri muda ulivyosogea na chachu ya Injili kuzidi kuenea, ilifika wakati Wakristo waliotoka Kowak na kuja Buturi, wakaanza kumsihi Padre ahamishie kanisa maeneo ya Kowak kwa sababu kuwa Buturi palikuwa pembezoni. Kwa jinsi walivyozidi kudumu katika ombi lao na pia kutokana na uaminifu wao, mwaka 1935, Askofu Oomen alikuja kujionea mwenyewe hali halisi. Alitoa kibali na hatimaye wamisionari walihamia kituo cha Kowak.

Msafara wa Askofu Oomen ulipofika maeneo ya Kowak kazi ya kwanza ilikuwa kutafuta maeneo ya kuishi na kuanzisha taasisi mbalimbali. Mtemi wa wakati huo , Yamo Odongo, alimpokea Askofu bila shida sana ila hofu yake ilikuwa ni juu ya ukubwa wa ardhi iliyoombwa na Baba Askofu. Baada ya kujaribu kutafuta ardhi katika maeneo ya Nyasoko, Dudu-Manyara na Rabuor, hatimaye ardhi ilipatikana maeneo ya Dudu ambayo ilitolewa na wenyeji, wakiwemo Mzee Jacob Okoth, Ojwang Ajuoga, na Omundu Odiero. Hapo Dudu ndipo lilipojengwa Kanisa, nyumba ya mapadre, shule, hospitali na nyumba ya masista.

Ujenzi ulianza rasmi mwaka 1935 na kukamilika mwaka 1937. Tayari kwa wakati huo, mapadri Ettiene Brussard na William walikuwa wamekwishahama kabisa kutoka Aheko Buturi kwenda Kowak tangu mwaka 1936, japo mwaka mmoja baadaye Pd. Brussard alirudi Nyegina na akaja Pd. Joseph Capps.

Missioni ya Kowak ilistawi kwa kasi kubwa, na ilipambwa kwa shughuli mbalimbali kama vile, Shule – iliyoanzishwa na Pd. Joseph Capps. Palikuwepo pia nyumba mbili kubwa kwa ajili ya wale waliotamani maisha ya Ubikira na wale wa Ubruda, wakatekumeni walioongezeka siku kwa siku hadi kufikia kama 500 hivi; wageni waliofika hapo siku kwa siku – wakiwemo wajane na wahitaji wengine. Kila siku ilitawaliwa na shamrashamra za aina mbalimbali, japo upinzani nao haukokosekana.

Baada ya miaka mitatu, Pd. Joseph Capps alihama toka Kowak na kurudi Nyegina, na baadaye kuhamia Seminari ya Nyegezi. Nafasi yake pale Kowak ilichukuliwa na Pd. Hendriks ambaye naye alikaa Kowak kwa miaka miwili na baadaye nafasi yake ikajazwa na Pd. Albert Scheven akifuatiwa na Pd. Matte, na baadaye mwaka 1939 Padri Erwin Binder (maarufu kama “abuoga”, maana yake - tishio) alitumwa Kowak ili asaidiane kazi na Pd. William Van Der Heidejen.

Kazi ya Uinjilishaji iliendelea, na mnamo mwaka 1942 lilitokea pigo lingine la kumpoteza Padre Brussard ambaye alifia Nyegina alikokuwa akiishi na akawa padre wa tatu kufia Nyegina. Hata hivyo kazi ya uinjilishaji ilizidi kusonga mbele, japo upinzani nao ulikuwepo toka kwa wale walioamini katika imani za jadi na pia toka kwa waamini wa madhehebu mengine ambayo yalikuwa yameanzishwa tayari katika maeneo ya Saye mnamo mwaka 1931.

Muda mfupi kabla ya mwaka 1946 Bruda Collect alirudi kwao na kutumwa Bruda Wilfred (wenyeji walimpa jina Ombajo) ili kuimarisha ujenzi. Idadi ya Wakristo-wabatizwa ilizidi kuongezeka siku hadi siku. Kufikia mwaka 1946 watu wapatao 8234 tayari walikuwa wamekwishabatizwa hapo Kowak.

SHIRIKA LA WAMISIONARI WA MARYKNOLL
Kundi la pili na la muhimu kabisa la Wamisionari, ambalo mchango wake mkubwa katu hauwezi kusahaulika, ni la Wamisionari wa Maryknoll. Shirika hili la kimisionari la Amerika, lilianzishwa na Pd. James Anthony Walsh.

Wamisionari wa shirika hili ndio waliwafuatia Mapadre wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, katika kueneza Imani ya Kikristo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara. Wanakumbukwa kwa namna ya pekee sana kwani ni katika kipindi chao ndipo Musoma imekua hatua kwa hatua hadi kufanyika kuwa Jimbo kamili. Vile vile Askofu wa kwanza wa Jimbo, Mhashamu John Rudin, alitoka katika shirika hili.

JITIHADA ZA AWALI ZA WAMISIONARI WA MARYKNOLL KUJA KUINJILISHA MARA
Padre wa kwanza kabisa wa Maryknoll kufika Tanzania (kwa wakati huo Tanganyika) alikuwa ni Pd. John Considine – aliyepata Upadre mwaka 1923, ambaye alifika Nyegina baada ya kufanya safari ndefu, iliyosukumwa na kiu yake ya kutamani kuja kuinjilisha Afrika, na hasa Tanganyika – ikiwemo Musoma.

Akiwa kama mwakilishi wa Baba Mtakatifu na wa Shirika lake pia, Pd. Considine alipeleka ripoti yake kwa Baba Mtakatifu PIO WA XI aliyekuwa Papa kipindi hicho, na pia ripoti kwa Wakuu wa Shirika lake, akitoa Wito kwa wenzake kuwa lipo hitaji kubwa la kuja kufanya umisionari Afrika.

Baada ya Ripoti yake, Wakuu wa Shirika la la Maryknoll – chini ya Askofu James Anthony Walsh waliazimia kuanzisha rasmi umisionari barani Afrika, hasa Afrika Mashariki, nchini Tanzania. Kwa namna hiyo, Pd. John Considine akawa chachu ya kweli iliyofanya kazi ya umisionari kwa Afrika iendelee kukua, na hata kushika kasi zaidi mwaka 1939 kulipozuka Vita vya Pili vya Dunia.

MUSOMA KUFANYIKA VICARIATE YA MUSOMA- MASWA NA KUKABIDHIWA KWA MARYKNOLL
Baada ya miaka kadhaa ya mazungumzano na mikakati, baina ya “Propaganda Fide” na “Maryknoll Superiors” ndipo tarehe 14 Februari, 1946 Shirika la Maryknoll lilipewa rasmi Vikarieti ya Musoma – Maswa iliyokuwa imezaliwa toka katika Vikarieti ya Nyanza.

Kwa kuanzia, mnamo tarehe 15.10.1946 Maryknoll waliwatuma Wamisionari wanne, na baadaye kutuma wawili wawili hadi kufikia mwaka 1950. Wanne waliotumwa kwanza ni: Pd. William J. Collins, Pd. Louis I Bayless, Pd. Albert E. Good na Pd. Joseph E. Brannigan. Mkuu wa Msafara alikuwa ni Pd. William Collins. Hawa wanne wa kwanza wanapotumwa ni wakati sasa imepita miaka karibu 15 tangu Pd. Considine alipotoa mwaliko kwa wenzake kuja kuinjilisha Afrika, mwaliko alioutoa baada ya yeye kuwa amefika Afrika na kujionea hitaji halisi.

Baada ya safari ndefu sasa, tena ya kuchosha, kutoka Amerika hadi Afrika, wamisionari hatimaye wanafika Musoma tarehe 23.10.1946 na kupokelewa na Pd. J. Van Riel aliyekuwa “Vicar Delegate” wa Askofu Joseph Blomjous ambaye alikuwa akiishi Mwanza.

Mnamo mwaka 1948, takribani miaka miwili baada ya Mapadri wa Maryknoll kuwa wamefika Musoma, walifika Masista wa Maryknoll kwaajili ya Misioni ya Kowak.

MUSOMA KUFANYIKA KUWA PREFEKTURA YA KITUME (“PREFECTURE APOSTOLIC”)
Mnamo tarehe 24 Juni, 1950 Musoma ilipewa hadhi ya kuwa “Prefecture Apostolic” na tarehe 07.07.1950 Kamati ya Papa ya Propaganda Fide iliwapa Wamisionari wa Maryknoll dhamana ya kuongoza Jimbo la Musoma ambalo kwa sasa lilikuwa limepata hadhi ya kuwa “Prefecture Apostolic” na Pd. William Collins akawekwa kuwa kiongozi wa muda, hadi ilipofikia tarehe 07 Desemba, 1950, ambapo Msgr. J. Gerard Grondin MM alipewa wadhifa wa kuwa “Prefect Apstolic.” wa Musoma.

Tangu mwaka 1952, Misioni ya Kowak ilibaki rasmi chini ya Mapadri na Masista wa Maryknoll baada ya Pd. Erwin Binder WF kuondoka Kowak na kuhamia Kome na baadaye Sengerema.

Kazi ya Wamisionari wa Maryknoll ilizidi kuzaa matunda, na kadiri ya muda parokia nyingi zaidi zilizidi kuanzishwa. Mnamo mwaka 1952 Pd. Edward Bratton, akitokea Kowak, alianzisha Parokia ya Komuge ambayo ilikuja baadaye kuendelezwa na Pd. Arthur Wille. Baadaye mwaka 1956 Pd. Glynn alianzisha Parokia ya Nyarombo na kuhamia huko; na baadaye kufuatiwa na Parokia ya Ingri iliyoanzishwa mwaka 1962 kwa jitihada za Pd. James Kuhn.

Kwa upande wa Miito ya Upadre, mwitikio kwa Wito wa Upadre haukuwa mkubwa. Matunda ya kwanza kwa parokia ya Kowak ni Pd. William Wasonga, Sr. Tereza, Sr. Consalva na Sr. Paschalia. Mapadre Alexander Choka na Tarcisius Sije, kwa kuzaliwa ni Nyarombo japo wanahesabika kuwa matunda ya Kowak kwavile walibatizwa hapo na pia waliisomea hapo Kowak.

UJIO WA MASISTA WA MARYNKOLL

Kwa mwaliko wa Pd. William Collins, mnamo Desemba 1948 MASISTA WA MARYKNOLL waliingia Musoma wakitokea Nairobi. Kundi la kwanza la Masista waliofika ni: Sr. Margareth Rose Winkelman, Catherine Maurine Bowes, Jean Michel Kirsh, Stanslaus Cannon. Hawa walikuja kwa ajili ya Utume Maalum, yaani: Kufungua Kituo cha Afya, Kuanzisha Shule ya Wasichana na pia kuwalea Masista wa Shirika la Moyo Safi wa Maria Afrika (IHSA).

MCHANGO WA MABRUDA WA SHIRIKA LA MARYNOLL

Katika shughuli nzima ya uinjilishaji iliyofanywa na Mapadre na Masista wa Maryknoll, hauwezi kamwe kusahaulika mchango wa Mabruda na Wamisionari Walei wa ki-maryknoll, ambao walifanya kazi bega kwa bega na mapadre na masista.

Kwa Upande wa Mabruda, unakumbukwa mchango wa pekee wa Br. Fidelis Diechelbohrer – ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kufika mnamo mwaka 1948. Yeye alikuwa ni fundi seremala, na anakumbukwa kwa kujenga na pia kukarabati majengo ya Kowak na Nyegina, na nyumba ya masista Kowak. Pia kwa kushirikiana na Br. Damian, walishiriki katika ujenzi wa Seminari ya Makoko. Anasifika sana kwa kuwa mwalimu mzuri kwa wenyeji juu ya taaluma ya useremala. Wengine wanaokumbukwa ni mabradha: John Damian Walsh, Brian Fisher, Peter Agnone (aliyeshirikiana na Bro. Brian kujenga Kanisa Kuu la na nyumba ya Askofu Rudin), Kelvin Dargan (aliyekuwa mwalimu wa vijana), John Frangenberg – ambaye alisaidiana na Pd. Arthur Wille kujenga Kituo cha Masista cha Baraki, na John Walsh (aliyesimamia ujenzi wa Kanisa la Tarime na Shule ya Lugha ya Makoko).

MCHANGO WA WAMISIONARI WALEI WA MARYKNOLL

Tukiwatazama Maryknoll Lay Missionaries, tunaliona kundi la kwanza likiwa ni la hawa wafuatao: Jeroy Hansen, Al Hagan, Tom Borer, David Ramse, Barbara Bechtold. Baadaye mwaka 1980 walifika – John Close na Roxanne ambao walikuwa walimu katika Semianri ya Makoko, mwaka 1982 walifika walei kutoka Hong Kong – China wakiwemo: Jessica Ho (aliyejishughulisha na Katekesi) na Elizabeth Woo (aliyekuwa Mkunga).

MUSOMA KUFANYIKA KUWA JIMBO

Mnamo tarehe 05 Julai, 1957 ndipo Musoma ilipotangazwa na kupewa hadhi ya Jimbo; na tarehe 03 Octoba, 1957, Msgr. John Rudin (MM) akatawazwa kuwa Askofu wa kwanza wa Musoma. Aliliongoza Jimbo la Musoma kama Askofu kwa muda wa miaka 22, tangu 1957 hadi 1979.

MAFANIKIO YA WAMISIONARI WA MARYKNOLL

1. Kuanzisha Parokia mbalimbali.
2. Kujenga Seminari Ndogo ya Makoko.
3. Kuanzisha Kituo cha Malezi ya Familia: Makoko Family Centre – kilichoanzishwa kwa jitihada za Pd. David Jones M.M na Sr. Magreth Monroe MM.
4. Kuanzisha Chuo cha Makatekista cha Komuge – kilichoanzishwa na Pd. Arthur Wille mnamo mwaka 1966.
5. Kuanzishwa kwa Shule ya Lugha: Makoko Language School – iliyoanziswa na Sr. Anita McWilliam (ambaye alikiongoza tangu 1964 hadi 1978).
6. Kudumisha MAHUSIANO mazuri na Serikali: Mapadre wa Maryknoll walikuwa marafiki wakubwa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mfano: Pd. William Collins ndiye aliyeshuhudia Ndoa ya Mwl. Nyerere na Maria Gabriel tarehe 24.01.1953. Kadhalika, mapadri Collins na Albert Nevins na John Considine ndio walitoa NAULI ya Mwl. Nyerere kutoka Ulaya kwenda Amerika kutetea Uhuru wa Tanganyika mbele ya Umoja wa Mataifa – March, 1955.
7. Kuanzishwa kwa Shirika la Watawa la IHSA - Mwaka 1953 – ambalo lililelewa na Masista wa Maryknoll chini ya Msgr. Gerald Grondin.
8. Kuanzishwa kwa Middle School – Kowak mwaka 1954 ambayo ilisimamiwa na masista wa Maryknoll hadi mwaka 1957.
9. Kuanzishwa kwa “Tanganyika Catholic Welfare Association” umoja ambao Katibu wake Mkuu wa Kwanza alikuwa ni Pd. Gerald Grondin (MM) hadi mwaka 1963 ambaye alipokelewa na Pd. Delbert Robinson, akifuatiwa na Pd. James Sangu – ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Askofu wa Mbeya.

Hali kadhalika unakumbukwa mchango mkubwa wa kitaifa wa Pd. Richard Hochwatt ambaye alikuwa Mwalimu na Mlezi katika Seminari za Makoko, Kipalapala na Segerea na baadaye kuwa Katibu wa Idara ya Kichungaji ya TEC; pia Pd. Francis Murray ambaye alikuwa Katibu wa Idara ya Kichungaji ya TEC hadi mwaka 1967 ambapo alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa “Bukumbi Pastoral Institute” – ambayo baadaye ilikuja kujulikana kama “Tanzania Pastoral and Research Institute” (TAPRI) Makao yake Makuu yakiwa kwanza Kipalapala Tabora na baadaye kuhamishiwa Dar es Salaam.

No comments: