Thursday, November 1, 2012

SABABU ZA KUADHIMISHA SINODI JIMBONI MUSOMA

Wapendwa wanafamilia ya Mungu, katika kikao cha kwanza cha kamati kuu ya maandalizi ya Sinodi, Baba Askofu Michael Msonganzila aliweka wazi sababu tisa zinazotufanya tuadhimishe Sinodi wakati huu. Tunapenda sasa wasomaji wetu wapendwa wazifahamu sababu hizi muhimu kwetu katika kuadhimisha Sinodi ya Jimbo letu la Musoma.



1. Miaka 50 ya Jimbo.
Mwaka 2007 Jimbo letu liliadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Itakumbukwa kwamba Jimbo letu lilianzishwa Julai 5, 1957. Kwa umri huo wa zaidi ya miaka 50 sasa, ni wakati muafaka kufanya Sinodi ya Jimbo ili kutathmini ukomavu wa Jimbo na kupanga mikakati ya kuliwezesha Jimbo kuendelea kusonga mbele.

2. Miaka 100 ya Ukristo Jimboni
Mwaka jana 2011 Jimbo letu liliadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Ukristo. Ni wakati muafaka sasa kufanya Sinodi ili kutathmini ni kwa kiasi gani Ukristo umezama na unazidi kuzama katika maisha ya wakristo Jimboni Musoma. Ni wasaa pia wa kutathmini ni kwa jinsi gani sisi pia tumeweza kueneza Injili tuliyoipokea kwa furaha kupitia kwa wamisionari. Kuifahamu historia ya Jimbo la Musoma bofya hapa.

3. Miaka 50 ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano
Mwaka huu 2012 ni mwaka wa 50 tangu kuanza kwa Mtaguso wa Pili wa Vatikano. Mtaguso huu ulioanza Oktoba 11, 1962 ulitoa mafundisho mengi na ya msingi kuhusu muundo wa Kanisa kwa ndani na namna linavyopaswa kuhusiana na malimwengu nje yake. Mafundisho haya pamoja na mapokeo hai ya Kanisa, ndiyo yanayoliongoza Kanisa na bado ni mafundisho mapya kwa maana kwamba baada yake hakuna bado Mtaguso Mkuu mwingine ulioitishwa. Kwa jinsi hii, mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano yanapaswa kuwa bayana kwa wakristo wote ili wayaelewe vema na kuyaishi. Sinodi yetu ya Jimbo itatupa nafasi ya kuyatafakari kwa kina mafundisho haya na kuyaweka bayana kwa waamini wote wa Jimbo la Musoma. Waweza kuzipata hati zote 16 za Mtaguso huo kwa kubofya hapa.

4. Sinodi ya Kwanza ya Afrika
Mwaka 1994 ilifanyika Sinodi ya Kwanza ya Afrika. Sinodi hii ilijikita katika suala la Uchungaji barani Afrika katika nyanja za Uinjilishaji, Utamadunisho, Mazungumzano (Dialogue), Haki na Amani pamoja na Njia za Upashanaji Habari. Kwa kuadhimisha Sinodi ya Jimbo, tunapenda kuzama katika mafundisho ya Sinodi ya Kwanza ya Afrika ili tuweze kutajirishwa nayo na kuona ni kwa jinsi gani tumeweza kuyatekeleza Jimboni kwetu. Mafundisho ya Sinodi hiyo yanapatikana katika Waraka wa Kitume Ecclesia in Africa Waweza kuusoma waraka huo kwa kubofya hapa.

5. Sinodi ya Pili ya Afrika
Mwaka 2009 ilifanyika Sinodi ya Pili ya Afrika. Sinodi hii, pamoja na kuendeleza mafundisho ya Sinodi ya Kwanza, iligusia changamto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika mintarafu Haki na Amani zinazopelekea matatizo kama vile mapigano, vita na uongozi mbaya. Kwa jinsi hii Sinodi ililenga kulihusisha Kanisa barani Afrika katika utume wa Upatanisho, Haki na Amani. Kwa kuadhimisha Sinodi Jimboni Musoma, tunapenda kuyaweka bayana kwa wanajimbo wote mafundisho ya Sinodi ya Pili ya Afrika na kutathmini ni kwa kiasi gani tunayatekeleza ndani ya mipaka ya Jimbo letu. Mafundisho ya Sinodi ya Pili ya Afrika yanapatikana katika Waraka wa Kitume Africae Munus wa Papa Benedikto XVI. Waweza kuusoma waraka huo kwa kubofya hapa.

6. Mafundisho ya Kanisa kuhusu Jamii
Kanisa linajihusisha na ustawi wa jamii kama mojawapo wa sehemu muhimu ya utume wake wa uinjilishaji. Mwaka 2005 Kanisa lilitoa chapisho la Mkusanyiko wa Mafundisho yake kuhusu Jamii. Katika kuadhimisha Sinodi ya Jimbo, tunapenda wakristo kote Jimboni wayaelewe kwa kina mafundisho haya na wafahamu kwamba katika mafundisho haya ya Kanisa kuhusu Jamii, kuna kanuni za kutafakari na miongozo ya utekelezaji; vitu ambavo ndivyo vya msingi kwa ukuzaji wa ubinadamu wenye mshikamano na uliokamilika. Kwa jinsi hii tutatekeleza wajibu wa kichungaji wa kuyatangaza na kuyaweka mafundisho haya bayana ili wanajimbo wote waelimishwe na waweze kuyaishi. Bofya hapa kupata chapisho la Mkusanyiko wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu Jamii.

7. Mwaka wa Imani
Baba Mtakatifu ametangaza kuwa Kanisa lote litaadhimisha Mwaka wa Imani kuanzia Oktoba 11, 2012 hadi Novemba 24, 2013. Mwaka huu wa Imani unaanza tarehe ambayo ni kumbukumbu ya miaka 50 tangu ulipofunguliwa Mtaguso wa Pili wa Vatikano. Tarehe hii pia ni kumbukumbu ya mwaka wa 20 tangu Katekisimu ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa rasmi. Tarehe ya kumalizika kwa Mwaka wa Imani ni siku ya Sherehe ya Bwana Wetu Yesu Kristo, Mfalme wa Ulimwengu. Lengo la Mwaka huu wa Imani ni kutoa mwaliko kufanya upya wongofu wa kweli kwa Bwana ili wakristo wote wajazwe furaha ya kuishi maisha ya Ushuhuda kwa Kristo Mfufuka katika ulimwengu wa leo. Mwaka huu utaambatana na maadhimisho mengi katika ngazi mbalimbali za Kanisa. Katika Jimbo letu tunauadhimisha Mwaka wa Imani ndani ya maadhimisho ya Sinodi ili kwa pamoja tuweze kuyafahamu makusudio yake, tuyatekeleze na tutajirishwe kwa wingi wa neema ziletwazo na maadhimisho hayo. Kupata taarifa zaidi kuhusu Mwaka wa Imani bofya hapa.

8. Miaka 20 ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki
Mwaka huu 2012, ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu Katekisimu ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa rasmi. Katekisimu hii ilichapishwa Oktoba 11, 1992. Katika Katekisimu hii kuna utajiri wa mafundisho ambayo Kanisa limeyapokea, limeyatunza na kuyatambulisha katika historia yake ya zaidi ya miaka elfu mbili. Kwa kuadhimisha Sinodi yetu ya Jimbo tunapenda kwa pamoja kuvumbua upya na kujifunza upya misingi ya mafundisho ya imani yaliyomo na kutoa uhakika kwa wanajimbo wote mintarafu maisha ya kiimani. Bofya hapa kupata chapisho la Katekisimu ya Kanisa Katoliki.

9. Askofu Jimbo kutathmini Uinjilishaji Jimboni
Askofu wa Jimbo letu, Mhashamu Michael Msonganzila, anaelekea mwaka wa tano tangu aliposimikwa kuwa mchungaji mkuu wa Jimbo la Musoma. Itakumbukwa kuwa Mhashamu Askofu Michael Msonganzila aliwekwa wakfu kuwa na kusimikwa kuwa Askofu wa Musoma Januari 20, 2008. Kwa utashi wake anapenda kufanya tathmini ya Uinjilishaji jimboni katika kipindi hiki cha miaka mitano ya uongozi wake. Namna nzuri na ya kufaa zaidi kufanya tathmini ni kupitia Sinodi ya Jimbo.

Hizo ndizo sababu tisa zinazotufanya tuadhimishe Sinodi Jimboni Musoma. Sinodi hii ni ya kwanza katika historia ya Jimbo letu. Tunaomba waamini wa Jimbo la Musoma na wote wenye mapenzi mema tushirikiane na tuunganishe nia zetu kuombea mafanikio ya Sinodi yetu ya Jimbo.



KUMBUKA
Unaweza kujipatia nakala ya vitabu vyote vilivyotajwa katika makala hii kupitia;

DUKA LA VITABU LA JIMBO
S.L.B 93
MUSOMA


Waweza pia kuagiza kupitia kwa Meneja; Pd. Alfred Kwene, Simu (+255 784 659707 au             +255 752 925806), Barua Pepe (kwenealfred@yahoo.com).

No comments: