Wednesday, May 15, 2013

VITENGE VYA SINODI VYAANDALIWA


Zikiwa zimesalia siku chache kufikia siku ya Uzinduzi wa Sinodi hapo Jumapili Mei 19, 2013, zoezi la kuandaa vitenge vya Sinodi limekamilika. Vitenge hivi vinategemewa kuwa sehemu ya vazi rasmi katika kipindi chote cha Sinodi na kubaki kama kumbukumbu ya tukio hili hata baada ya Sinodi mwisho wa mwaka 2014. Alama zilizopo kwenye kitenge hicho ni pamoja na Nembo ya Mwaka wa Imani, kauli mbiu ya Sinodi (Imani na Matendo) na mchoro wa samaki ambao ni mojawapo wa vielelezo asilia vya mkoa wa Mara lililoko Jimbo la Musoma.

Vitenge hivyo vimetengenezwa na Shirika la Masista wa Moyo Safi wa Maria Afrika, taasisi iliyokabidhiwa jukumu hilo na Kamati Kuu ya Maandalizi ya Sinodi. Akizungumza wakati wa kuvionesha vitenge hivyo mapema leo, Mama Mkuu wa Shirika hilo Sr. Lucy Magumba alieleza kuwa vitenge hivyo vimeandaliwa kwa ubora wa hali ya juu na kwa kuzingatia vionjo vya watumiaji. “Kitenge ni kipana na chenye uzito unaofaa kabisa…. Rangi ni nzuri kabisa na tumeandaa kwa rangi tatu tofauti ili kila mmoja achague rangi anayopendelea zaidi” alieleza Mama Mkuu huyo na kuongeza kuwa kutokana na ubora wake watu waweza kushona mashati au makoti hasa kwa akinababa na aina nyinginezo za mavazi kwa akinamama.
Sr. Lucy Magumba, Mama Mkuu IHSA akionesha sampuli ya vitenge vya Sinodi

Vitenge vitapatikana katika kipindi chote cha Sinodi. Wakazi wa Musoma waweza kununua vitenge hivyo kutoka katika duka la vitabu la Jimbo lililoko jengo la RC Conference Centre. Walio nje ya Musoma na wengineo waweza kuagiza kutoka Makao Makuu ya Shirika IHSA. Kwa mawasiliano: Sr. Stella Matutina 0752 225 771.


1 comment:

Anonymous said...

HAKIKA KITENGE NI KIZURI.
HONGERA WANA IHSA KWA KAZI NZURI.