Wednesday, June 5, 2013

VIKAO VYA SINODI VYAANZA


Baada ya uzinduzi rasmi wa Sinodi katika Dominika ya Pentekoste, 19 Mei 2013, awamu ya kwanza ya vikao vya Sinodi yaanza. Awamu hii inajumuisha vikao vinavyofanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 03 Juni hadi 07 Juni. Vikao hivi vinafanyika katika kituo cha Jimbo cha Sala na Mafungo, Epheta.

Mada kuu inayojadiliwa katika kikao hiki ni UINJILISHAJI. Mada hii itajumuisha, miongoni mwa mengine, Katekesi, Sakramenti, Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na Wadau wa Uinjilishaji. Wajumbe wa Sinodi wamehudhuria kwa wingi isipokuwa wachache walio na udhuru.

Leo kikao hicho kimeingia siku ya tatu baada ya ufunguzi uliofanywa na Askofu wa Jimbo, Mhashamu Michael Msonganzila juzi tarehe 03 Juni. Katika siku hizi tatu tayari vipengele kuhusu Katekesi na Sakramenti vimejadiliwa. Muwezeshaji wa mada hizo ni Pd. Raphael Madinda, Katibu wa Idara ya Katekesi Baraza la Maaskofu Tanzania.

Kadiri ya utaratibu wa jumla wa uendeshaji wa Sinodi, kikao hiki kinalenga kujadili hoja zinazoibuliwa na madodoso yahusuyo mada iliyopo mezani. Mijadala hii ndiyo itakayozaa mapendekezo yatakayopigiwa kura na yakisha pitishwa na Askofu wa Jimbo yatakuwa maamuzi ya Sinodi ya Jimbo.

Tunaendelea kuikabidhi Sinodi chini ya Maongozi ya Mwenyezi Mungu kwa maombezi ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, msimamizi wa Jimbo letu.

No comments: