Tuesday, March 5, 2013

SEMINA ELEKEZI YA SINODI YA JIMBO

Tarehe 21 na 22 Januari 2013 ilifanyika semina elekezi ya Sinodi ya Jimbo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwembeni. Wawezeshaji katika semina hiyo walikuwa ni Pd. Romuald Kajara wa Jimbo la Rulenge - Ngara na Pd. Laurenti Magesa wa Jimbo la Musoma.

Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila wakati wa ufunguzi wa semina hiyo. Hotuba ya Baba Askofu ilieleza maana na malengo ya sinodi kwa ujumla pamoja na sababu za kuadhimisha sinodi katika jimbo la Musoma.



 UTANGULIZI:
 Wapendwa mapadre, watawa, walei na watu wenye mapenzi mema, wapendwa wageni waalikwa, (kwa namna ya pekee Mwezeshaji wetu Pd. R. Kajara), na waamini wote wa Jimbo Katoliki la Musoma, Neema na Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo viwe nanyi nyote.
 

Ninapenda kuchukua nafasi hii kutoa Neno langu la Ufunguzi rasmi wa Semina hii – ambamo nitaeleza maana ya Sinodi, Malengo, maadhimisho na Sababu wa kuwa na Sinodi na mategemeo ya Sinodi. Ninaomba usikivu wenu ili haya nitakayoyaeleza yaweze kueleweka vema na yatusaidia tunapoanza rasmi safari yetu ya kuadhimisha sinodi yetu ya Jimbo.
 

 SINODI YA JIMBO NI NINI?
 Ni Mkutano unaoitishwa na Askofu wa Jimbo. Unajumuisha Mapadre,watawa, na walei wanaoteuliwa kwa ajili ya kumsaidia Askofu wa Jimbo katika kuboresha hali ya maisha utume wa Kanisa kama “Familia ya Mungu”. (kadiri ya Mtaguso wa Pili wa Vaticano). Neno “Sinodi” linatokana na Neno la Kigiriki - σύνοδος (synodos) linalomaanisha “mkutano” au mkusanyiko ("assembly" or "meeting").

  Kadiri ya HATI YA SHERIA KANUNI ZA KANISA YA MWAKA 1917, kila baada ya miaka 10 iliagizwa ifanyike Sinodi ya Jimbo na kwa wakati huo ilihusisha Mapadre tu (kadiri ya muono wa Vaticano ya I)


 MALENGO YA SINODI:

  •  Sehemu ya kwanza ya malengo ya sinodi inahusisha masuala ya maisha yetu kama Wakristo, yaani, wafuasi wa Kristo, na washiriki katika Ujenzi wa Ufalme wa Mungu mioyoni mwa ndugu zetu, ambayo ni pamoja na: kusali pamoja, kutafakari pamoja, kupanga pamoja, kutathimini pamoja.   
  •  Kuibua mawazo, kuyajadili na kuyatolea mapendekezo yenye mwelekeo wa kiutendaji katika utume wa Kanisa Jimboni Musoma.
     
  •  Kutazama tulikotokea, tulipo na tunapoelekea kiuchungaji, ki-uchumi, kiutendaji na maadhimisho ya Liturujia ili kukirithisha kizazi kijacho katika Imani ya Kikristo.
     
  •  Kujitengenezea “METANOIA”, yaani, mabadiliko ya kina, ya ndani kabisa kadiri ya Neno la Mungu na taratibu za Kanisa – kujiwekea MOYO WA NYAMA.

 ADHIMISHO LA SINODI:
Kulingana na Sheria Kanuni za Kanisa, ni Askofu wa Jimbo pekee ndiye mwenye dhamana ya kuitisha Sinodi katika Jimbo lake (Can. 462 § 1). NI himizo la Kanisa kuwa kila Jimbo lifanye Sinodi baada ya kipindi fulani, na ni Askofu wa Jimbo baada ya kushauriana na Baraza la Mapadre, ndiye anayeamua ni wakati upi ulio muafaka kwa Jimbo lake kuwa na Sinodi (Can. 461 § 1)..

Kwa tafsiri hiyo iliyoelezwa hapo juu, baada ya kushauriana na kupata ridhaa ya Baraza la Mapadre, kwetu wanajimbo la Musoma wakati huu ninauona kuwa ndio wakati muafaka wa kufanya Sinodi yetu ya Kwanza ya Jimbo. Ninapenda kuainisha sasa sababu msingi zinazonifanya niuone wakati huu kuwa ndio wakati muafaka kwetu kuwa na Sinodi ya Jimbo kama ifuatavyo:


V. SABABU ZA KUWA NA SINODI YA JIMBO LA MUSOMA: 2013/ 2014

  •  Miaka zaidi ya 100 ya Uinjilishaji: Nawaalika wote tuliomo kwenye ukumbi huu, tuendelee kumshukuru Mungu kwa zawadi ya UHAI NA IMANI YA KIKRISTO. Katika Jimbo la Musoma, Imani ya Kikristo imekuwepo humu tangu mwaka 1911. Ni mwaka 2011 tumeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu habari njema kuhubiriwa katika eneo hili.
  •  Mwaka 2007 tuliadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo wa Jimbo Katoliki la Musoma. Matukio yote haya mawili yanatupatia fursa ya kujiandaa kikamilifu kuitafiti kwa kina Historia ya Jimbo letu tukianzia na Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) waliofika kwanza eneo hili, na baadaye kufuatiwa na Shirika la Wamisionari wa Maryknoll. Iko haja ya kutamani sana kwa macho, masikio na kiimani kurithisha na kuendeleza jitihada za mwanzo za uinjilishaji wa wamisionari wa Afrika na pia wamisionari wa Maryknoll.
  • Miaka 50 ya Mtaguso wa II wa Vaticano: Historia ya Kanisa miaka 50 iliyopita inatufundisha kuwa mnamo tarehe 11 Oktoba,1962, Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII, aliitisha MTAGUSO MKUU WA PILI WA VATICANO ambao ulisisitiza sana kuwa KANISA LIJITATHIMINI UPYA, LIJIREKEBISHE UPYA, LIJITAZAME UPYA, LIJICHUNGUZE, LIFANYE MAREKEBISHO NA MAGEUZI HALALI KUENDANA NA HALI HALISI YA ULIMWENGU WETU WA LEO. Kutokana na umuhimu wake nitaieleza kirefu:
Ili kukidhi adhima hiyo, Mtaguso wa Pili wa Vaticano katika majadiliano yake ulifanikiwa kuchapisha na kusambaza HATI 16 za Mafundisho yaliyojaa utajiri kwa kiimani, maadili na nidhamu ndani ya Kanisa lote. Hati hizi zimegawanyika kama ifuatavyo:

1) Hati Nne za kwanza za Mtaguso wa Vatican II zinaitwa KATIBA ZA MAFUNDISHO MUHIMU YA KANISA (CONSTITUTION):

(i) LUMEN GENTIUM: - “Mwanga wa Mataifa” – yaani, Kanisa Katoliki linajitambulisha kuwa ni Mwanga wa Mataifa.
(ii) DEI VERUBUM: - “Neno la Mungu” – yaani, Kanisa ni Jumuiya inayosimikwa katika Ufunuo wa Neno la Mungu.
(iii) SACROSANCTUM CONCILLIUM: - yaani, Kanisa ni Jumuiya inayoabudu hasa kwa adhimisho la Sakramenti ya EKARISTI TAKATIFU. Hati hii inatufundisha daima kutambua kuwa LITURUJIA NI NIDHAMU YA UTARATIBU MAALUM WA KANISA KATIKA IBADA NA MAADHIMISHO YAKE MBALIMBALI.
(iv)GAUDIUM ET SPES: - yaani, FURAHA NA MATUMANI: Hati hii inalitambulisha Kanisa kuwa ni chombo cha wokovu chenye kuleta furaha na matumaini kwa wanadamu ulimwenguni.

Wapendwa wajumbe, hati hizi nne zinaeleza kwa kina na mapana katika lugha nyepesi juu ya NIA NA LENGO la Utashi wa Yesu Kristo kwa Kanisa lake.

Hati hizi nne za Kikatiba, zinatualika na kutuagiza kuondoa kabisa yale mambo yasiyo ya lazima katika Ukristo wetu kusudi UINJILISHAJI UONEKANE WAZI KATIKA JAMII YETU INAYOKUWA KATIKA MAZINGIRA NA MABADILIKO MENGI YA KILA WAKATI.

2) Kundi la Pili la Hati hizi linaitwa MAAZIMIO MATATU YA MTAGUSO WA PILI WA VATIKANO:
(i) Azimio la Kwanza linahusu: “UMUHIMU WA ELIMU” – “Gravissimum Educationis”
(ii) Azimio la Pili linahusu: “UHUSIANO WA KANISA NA DINI ZINGINE ZISIZO ZA KIKRISTO” – “NOSTRA AETATE”
(iii) Azimio la Tatu linahusu: “UHURU WA MTU KATIKA SWALA JUU YA KUABUDU” – “DIGNITATIS HUMANAE”

3) Kundi la Tatu la hati hizi ni MATAMKO MATATU JUU YA KUBADILI MIOYO YETU:
Matamko haya yanatutayarisha na kutusaidia kuweka tayari mioyo yetu ili tuweze kweli kupokea mafundisho ya Kanisa.
(i) Vyombo vya Upashanaji Habari: - “INTER MIRIFICA”
Kanisa lipinge mila na desturi potovu za giza zinazoweza kusambazwa na vyombo vya mawasiliano na upashanaji habari na badala yake vyombo hivyo hivyo vitumike katika kueneza UFALME WA MWANGA.
(ii) Makanisa ya Mashariki – “ORIENTALIUM ECCLESIARUM”
Jitihada njema za Makanisa ya Mashariki katika kuboresha Liturujia na kuendeleza Elimu ya Teolojia tangu mwanzo wa Ukristo ziendelezwe.
 Makanisa haya ni sehemu ya ya Kanisa Katoliki.
Jitihada za kuyafikia makanisa mengine ya mashariki ziendelezwe.

(iii) UHUSIANO WA KIDUGU WA MAKANISA MENGINE YA KIKRISTO AMBAYO SI YA KIKATOLIKI – “UNITATIS REDINTEGRATIO” – EKUMENE. 

Kuimarisha mahusiano mema kati yetu wakristo na kuudumisha.

4) MATAMKO SITA YA MTAGUSO JUU YA MAENEO MAALUM YA KUREKEBISHWA:
Lengo ni kuleta mageuzi, mabadiliko katika Kanisa kadiri ya majukumu ya wanakanisa wote.

(i) WAJIBU WA MAASKOFU – “CHRISTUS DOMINUS”
(ii) KUHUSU MALEZI YA SEMINARI – “OPTATAM TOTIUS”
Malezi bora katika Seminari zetu na jinsi ambavyo kila mmoja anaalikwa kushiriki.

(iii) KUHUSU MAISHA YA HUDUMA YA MAPADRE: - “PRESBYTERORUM ORDINIS”:- Malezi bora ya upadre – kielimu na kimaadili
 Kukuza ushirikiano katika huduma yao ya kichungaji.

(iv) MAISHA YA WAKFU KATIKA KANISA:- “PERFECTAE CARITATIS”
Nafasi ya Watawa katika Kanisa tuifahamu vema
Ushirikiano wetu na Watawa uongozwe na taratibu zilizowekwa na Kanisa.

(v) UMISIONARI WA KANISA: - “AD GENTES”
 Mwaliko wa Mtaguso wa Pili wa Vatikani kwa kila mbatizwa kuwa mmisionari.
Tutolee nguvu zetu zote kwa ajili ya maendeleo ya ustawi wa Kanisa.
Tujitoe sadaka sisi wenyewe.

(vi)UTUME WA WALEI:
 Nafasi ya Walei ndani ya Kanisa
 Kusimika familia za kikristo zilizo misingi ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo.
 Kutakatifuza ulimwengu kwa kuonesha ushuhuda wa kina katika nyanja mbalimbali.
 Kuiga mfano wa familia ya NAZARETI.


  •  SINODI MBILI ZA MAASKOFU KWA AJILI YA BARA LA AFRIKA NA MADAGASCAR:
 Kati ya miaka ya 1994 na 2009, pamekuwepo na Sinodi mbili za Maaskofu zilizojadili mambo muhimu yanayolihusu Kanisa la Afrika na Madagascar.
 Mambo yaliyoongelewa na kuamuliwa katika Sinodi hizi ni mengi na ya maana sana kwa Kanisa letu la Afrika – Jimbo la Musoma likiwemo.
 

  •  MWAKA WA IMANI:
Mwaka 2012/13 umetangazwa kuwa Mwaka wa Imani – ambao rasmi unaadhimishwa kuanzia tarehe 11 Oktoba 2012 hadi 24 Novemba, 2013.  Lengo Kuu ni kuamsha katika kila muumini hamu ya KUKIRI IMANI KIKAMILIFU NA KWA UTHABITI MPYA, KWA KUJIAMINI NA KWA MATUMAINI.
 Mwaka unaotupatia fursa kubwa sisi sote kukuza ushuhuda wa maisha yetu katika IMANI tunayosadiki katika mazingira yetu.
 Tuamini kwa moyo, na tukiri kwa kinywa.

  • KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI:
 Ni miaka ISHIRINI sasa imetimia tangu itangazwe rasmi na Mwenyeheri Yohane Paulo II (11 Oktoba, 1992) Katekisimu hii ni tunda kuu la pili la Mtaguso wa Pili wa Vatikano.

  • SHERIA ZA KANISA – C.I.C. (1983 – 2013)
Imetimiza miaka 30 tangu itangazwe rasmi tarehe 25 Januari, 1983.
  •  MIAKA MITANO (5) YA UASKOFU:
Jana tu, tarehe 20 Januari, 2013 nimetimiza rasmi miaka mitano ya uaskofu. Kipindi hiki kimenifundisha mengi juu ya Uchungaji na Maendeleo ya Jimbo letu.
Ni vizuri tushirikishane hayo na hatimaye kuyaweka kama sehemu ya maazimio yetu.



VI. HATUA TULIYOFIKIA HADI SASA KATIKA MAANDALIZI YA SINODI YETU YA JIMBO:

Wapendwa washiriki wa Semina hii Elekezi, na ambao pia ndio mtakuwa WAJUMBE RASMI WA VIKAO VIJAVYO VYA SINODI mlioko hapa, ninapenda pia kutumia nafasi hii kuwashirikisheni hatua ambazo tumekwishafikia hadi sasa katika maandalizi ya Sinodi yetu ya Jimbo kama ifuatavyo:

1. Tangazo rasmi la Nia ya kuwa na Sinodi ya Jimbo (sio kwa maandishi): Tayari nilikwishatoa tangazo rasmi na kueleza kwa ufupi sababu za kuwa na sinodi yetu ya kwanza ya Jimbo – siku ya tarehe 12 Julai, 2012 katika Tukio la Upadrisho katika Kanisa Kuu la Jimbo la Musoma.

2. Uteuzi wa Kamati ya Maandalizi ya Sinodi - iliyotangazwa rasmi tarehe hiyo hiyo 12 Julai, 2012.

3. Kikao cha Kwanza cha Ufunguzi wa Kamati ya Maandalizi ya Sinodi – tarehe 28 Agosti, 2012.

4. Kuundwa kwa Kamati Ndogondogo kutokana na Kamati Kuu ya Maandalizi, ambazo ni:
a) Kamati ya SALA YA SINODI, KAULI MBIU NA WIMBO WA SINODI.
b) Kamati ya UKUSANYAJI MADODOSO (yanayohusu masuala ya kichungaji) toka Parokiani
c) Kamati ya Fedha
d) Kamati ya Mawasiliano
e) Kamati ya kutengeneza MWONGOZO (Directory) ya Sinodi ya Jimbo.

5. Ukusanyaji wa Awali wa MADODOSO mbalimbali kuhusu masuala msingi ya kichungaji ambayo tungependa yajadiliwe katika Sinodi yetu ya JIMBO: Tayari baadhi ya madodoso yalikwishakusanywa na ndiyo hayo yatakayotusaidia katika kuandaa “madodoso rasmi” yatoakayotolewa ufafanuzi na maelekezo katik Semina ya leo.

6. Tayari tumekwishatunga KAULI MBIU YA SINODI, ambayo ni: “SINODI MUSOMA: IMANI NA MATENDO”

7. Mwongozo (directory) ya Sinodi: Kwa kupitia Kamati ya Mwongozo iliyoainishwa hapo juu, tayari tumekwishaandaa MWONGOZO (Directory) wa Sinodi – ambao unaainisha RATIBA YA VIKAO VYA SINODI na MADA ZITAKAZOJADILIWA katika VIKAO VIJAVYO VYA SINODI.

8. Uteuzi wa Washiriki (wajumbe) wa Vikao vya Sinodi ya Jimbo, na tayari wamekwishapewa barua za uteuzi wao na ndio hawa tunaohudhuria Semina hii Elekezi siku ya leo na Kesho.


VII. SEMINA ELEKEZI INAYOFANYIKA LEO TAREHE 21 JANUARI NA KESHO TRH. 22 JAN., 2013:
Baada ya kuwa tumepitia hatua hizo mbalimbali katika maandalizi ya Sinodi yetu ya Jimbo kama ilivyoainishwa hapo juu, ilionekana ni vema kuwa na Semina Elekezi kwa Washiriki wote wa Sinodi ili kupata maelekezo ya msingi juu ya nini maana ya Sinodi na nini tunatakiwa kufanya katika Maandalizi ya Sinodi, wakati wa Sinodi na baada ya Sinodi.

Ndio maana tumekusanyika hapa katika siku hizi mbili kwa lengo hilo muhimu. Tumelazimika kuacha shughuli zetu na pia makazi na maeneo yatu ya kazi na kuja hapa kwa lengo hili maalum.

Ninapenda kuchukua nafasi hii, kwanza kabisa kumshukuru Mwezeshaji wetu – Padre Romuald Kajara wa Jimbo la Rulenge – Ngara, kwa kukubali mwaliko wetu na kuja Musoma kwa ajili ya utume huu muhimu. Ninamkaribisha pia Pd. Laurent Magesa – Padre Mwanajimbo, ambaye pia anashiriki katika Semina hii Elekezi. Ninawakaribisha sana Jimboni Musoma tukitumaini kuwa watatutajirisha vya kutosha, na tutakapotoka hapa basi safari yetu ya maandalizi ya sinodi na baadaye sinodi yenyewe itakuwa rahisi.

Aidha, ninamualika kila mmoja wenu katika Semina hii muhimu, nikiomba ushiriki ulio makini kutoka kwa kila mmoja wenu, tukijua kuwa baada ya Semina hii basi sote tunategemewa twende tukawe waalimu kwa wenzetu tuliowaacha huko nyumbani, ili mwisho wa siku Sinodi yetu imguse kila mwanafamilia ya MUNGU Jimboni mwetu MUSOMA.



NINAWATAKIA KILA LA HERI KATIKA SEMINA HII, NA MUNGU AWABARIKI NYOTE.

“SINODI MUSOMA – IMANI NA MATENDO”


No comments: